Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ametishia kutangaza vita dhidi ya Rwanda Jumatatu wakati wa mkutano wake wa mwisho wa kampeni za uchaguzi mjini Kinshasa.
Akizungumza mbele ya maelfu ya wafuasi wake, Tshisekedi alisema “ikitokana na risasi ya kwanza iliyofyatuliwa, nitaitisha kikao cha bunge kwa sababu katiba inaniruhusu mimi kufanya hivyo, na nitatangaza vita dhidi ya Rwanda.”
Wanasiasa wa Congo na makundi mbalimbali likiwemo la waasi wa M23, ambao wameteka eneo la mashariki mwa DRC, na Corneille Nangaa, mkuu wa zamani wa tume ya uchaguzi ya Congo, walizindua ushirika wa Congo River Alliance huko Nairobi, Kenya Ijumaa.
Nangaa, ambaye aliwekewa vikwazo na Marekani kwa ufisadi na kuingilia uchaguzi wa 2018, alisema muungano huo utavileta pamoja vikundi mbalimbali venye silaha vya Wakongo, wanamgambo, na jumuiya za kijamii na kisiasa.
Hali ya kutokuwepo usalama ni sehemu ya athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyokuwa havijatafutiwa ufumbuzi ambavyo vilimalizika rasmi mwaka 2003.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya M23 yamechochea mivutano ya kidiplomasia na nchi jirani ya Rwanda, ambapo DRC na wataalam wa UN wanaishutumu kwa kuwaunga mkono wanamgambo hao. Rwanda inakanusha kuhusika.
Tshisekedi anachuana na takriban darzeni mbili za wapinzani katika uchaguzi mkuu siku ya Jumatano, Disemba 20. Wapinzani wake ni pamoja na hasimu wa kisiasa wa zamani kama Martin Fayulu, ambaye alitwaa nafasi ya pili katika uchaguzi uliokuwa na utata wa 2018, na mshindani mwengine ni Mshindi wa Tuzo ya Nobel Dr. Denis Mukwege.
#drc #rwanda #congo #felixtshisekedi #tshisekedi #drcelection #drcelection2023 #voa