Ukraine yaharibu meli kadhaa za Russia kwa makombora ya masafa marefu

  • | VOA Swahili
    387 views
    Majeshi ya Ukraine yameishambulia meli ya Russia iliyokuwa inawasili Crimea, shambulizi lililopiga sehemu ya meli kadhaa za Russia zilizoko katika bahari ya Black Sea ambazo jeshi la anga la Ukraine lilisema zinashukiwa kubeba droni zilizotengenezwa Iran. Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisema kuwa shambulizi lililofanywa na Ukraine liliharibu meli ya Novocherkassk katika kituo cha Feodosia. Sergei Aksyonov, gavana wa Crimea aliyewekwa na Russia, alisema kupitia mtandao wa Telegram shambulizi hilo liliuwa mtu mmoja na kujeruhi wengine wawili. Mashirika ya habari ya Russia yaliripoti kuwa Rais Vladimir Putin alipewa muhtasari wa shambulizi hilo. Jeshi la anga la Ukraine lilisema limetumia makombora ya masafa marefu na kuwa shambulio hilo liliiteketeza meli hiyo. Kamanda wa jeshi la anga la Ukraine Mykola Oleshchuk alisambaza video kupitia mtandao wa Telegram ikionyesha mlipuko mkubwa huko Feodosia. “Na meli za Russia zinazidi kupungua zaidi,” Oleshchuk alisema. Jeshi la Ukraine pia limeripoti Jumanne kuangusha droni 13 kati ya 19 ambazo zilitumiwa na Russia kufanya mashambulizi usiku kucha. Lilisema droni hizo ziliangushwa huko katika mikoa ya Odesa, Kherson, Mykolaiv na Khmelnytskyi Russia ilidai Jumatatu kuwa majeshi yake yalikuwa yameteka mji wa kimkakati wa Maryinka ulioko mashariki mwa Ukraine, lakini Kyiv ilikanusha dai hilo, ikiripoti kuwa majeshi yake yalizima “mashambulizi matatu yaliyofeli” karibu na jamii ambayo imeharibiwa na kutelekezwa. “Si sahihi kuzungumzia kuiteka Maryinka,” msemaji wa jeshi la Ukraine Oleksandr Shtupun alikiambia kituo cha televisheni cha Ukraine kufuatia madai ya Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu wakati wa mkutano wake na Rais Vladimir Putin ulioonyeshwa kupitia televisheni. “Mapigano yanaendelea huko Maryinka,” Shtupun alisema. “Hivi sasa, wanajeshi wetu wako katika maeneo ya utawala ya mpakani huko Maryinka, lakini mji huo umeangamizwa kabisa,” alisema. Waliochangia katika ripoti hii ni Radio Free Europe/Radio Liberty Baadhi ya taarifa katika ripoti hii zinatokana na mashirika ya habari ya Associated Press, Agence France-Presse and Reuters. #rais #vladimirputin #uhaini #wagner #usaliti #russia #joebiden #marekani #wagnergroup