Akitumia feni ambazo ameziokota kutoka soko la vifaa vya zamani na kuzizungushia nyaya, kijana Hussam Al-Attar ametengeneza chanzo chake mwenye cha umeme kuleta mwanga katika hema ambapo yeye na familia yake wanaishi baada ya kulazimika kukimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya Israel huko Gaza.
“Tulikimbia kutoka Kaskazini kuja Rafah, katika kambi hii, tukakaa siku 20 katika kiza, ilikuwa kiza kabisa wakati wa usiku, na nilikuwa nawasikitikia mama, baba na ndugu zangu kutokana na kiza totoro hapa, Kwa hiyo nikaja na fikra hii (ya kutengeneza mfumo wa umeme) kupunguza matatizo ambayo tunapitia wakati wa vita,” alieleza Al-Attar.
Kwa kutambua kipaji chake, watu katika eneo hilo la kambi yenye mahema wamempa jina la utani: Newton wa Gaza.
“Walianza kuniita Newton wa Gaza kutokana na vitendo vyangu kufanana na vya Newton,” alisema Al-Attar, ambaye anaonekana ni mdogo zaidi kwa maumbile na sauti kwa umri wake wa miaka 15.
Newton alikuwa amekaa chini ya mti wa matufaha wakati tufaha lilipodondoka kichwani na yeye kugundua nguvu za mvutano. Na sisi hapa tunaishi katika kiza na maafa, na roketi zinaanguka juu yetu, hivyo nilifikiria kutengeneza mfumo wa umeme, na nikafanya hivyo,” Al-Attar.
Mwanasayansi wa Uingereza Isaac Newton, ambaye alipiga hatua mbalimbali za kisayansi ikiwemo fizikia, hisabati na elimu ya sayari mwisho wa karne ya 17 na mwanzo wa karne ya 18, aliyepata umaarufu kwa fikra yake iliyoenea kutokana na hadithi ya tufaha, ambayo aliieleza mara kwa mara.
Zaidi ya nusu ya watu milioni 2.3 wanaoishi Gaza hivi sasa wamejazana huko Rafah, katika eneo la ukingoni kusini mwa Gaza ambao wanatenganishwa na wigo na Misri. - Reuters
Mashambulizi ya angani na ardhini yanayofanywa na Israel yameuwa watu karibu 27,000 na kujeruhi zaidi ya wengine 65,000 katika eneo finyu la Gaza.
Mashambulizi haya yalianza Oktoba 7 kufuatia mauaji ya Oktoba 7 huko kusini mwa Israel, yaliofanywa na wanamgambo kutoka Gaza waliouwa takriban watu 1,200 na kuwateka watu 250. - AP
#Haifa #waelaldahdouh #hamzaaldahdouh #shirikalamwezimwekundu
#Rafah #Netanyahu #Misri #Hamas #Gaza #Palestina #IDF #GalMeirEizenkot #mauaji #jeshi #israel #voa #voaswahili #mwandishi #aljazeera #maghazi #wahouthi #marekani #uingereza #shambulizi #dhamar #yemen #iran