Wananchi wa Haiti katika mji mkuu wa Port-au-Prince na vitongoji jirani wako mbiyoni wiki nzima hivi sasa bila ya kujuwa wapi watakwenda kutokana na mapigano kati ya magenge ya uhalifu na polisi.
Ghasia hiso zilizuka wiki moja iliyopita na kuilazimisha serikali kutangaza hali ya dharura, na Marekani kuwaondoa raia wake kuanzia Jumapili.
Hali katika nchi hiyo ya Caribean inaripotiwa kuwa mbaya sana na kuisababisha Jumuiya ya kimataifa kueleza wasi wasi wake na kutoa wito wa kusitisha ghasia na kudumisha amani.
Wakazi wa mji mkuu wa Port-au-Prince wanazidi kukabiliwa na hali mbaya ya maisha bila ya chakula, maji wala mahali yakuishi kutokana na mapigano ya magengi yanayoendelea kwa zaidi ya wiki moja sasa kati ya magengi ya wahuni na polisi.
Filienne Setoute ameliambia Shirika la Habari la AFP kwamba amefanya kazi kwa miaka 20 katika wizara ya huduma za jamii na ajira, na kuweza kujijengea nyumba yake, lakini hivi sasa hana tena mahali ya kulala.
Filienne Setoute mfanyakazi wa wizara ya huduma za jamii:
“Hatujaweza kulala kwa siku mbili hivi sasa. Tunakimbia, mimi na vitu vyangu kichwani bila ya kujuwa ninakwenda wapi. Nilikua na nyumba yangu lakini sasa sina makazi tena.
Kilio hicho kinaelezwa na mamia ya Wahaiti waliokuwa wanakimbia wakilaumu polisi kushindwa kufanya kazi zao.”
Reginald Bistol raia aliyepoteza makazi yake anasema:
“Hapa ni suala la kufa au kupona, hatuna la kufanya, hakuna tofauti kati ya nyumba za watu binafsi na mali ya umaa. Hebu fikiria, tukiuliwa sote hapa Port-au-Prince, haya majengo yatakua na maana gani? Wahuni wametulazimisha kuondoka kutoka makazi yetu, tumepoteza kila kitu tulokua nacho, tumepoteza familia. Sasa tuko barabarani.”
Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM limesema mwishoni mwa wiki kwamba karibu Wahaiti laki tatu elfu sitini na mbili wamekoseshwa makazi tangu kuzuka kwa ghasia hizi. - VOA, AFP, AP, Reuters
#haiti #magenge #polisi #wananchi #mauaji #wakimbizi #voa #voaswahili #carribean