Vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) vilizuia jaribio la mapinduzi lililohusisha wapiganaji wa Congo na wa kigeni Jumapili asubuhi, msemaji wa jeshi hilo alisema katika hotuba yake iliyopeperushwa kwa njia ya televisheni.
"Jaribio la mapinduzi limezimwa na vikosi vya ulinzi na usalama. Jaribio hilo lilijumuisha wageni na Wakongo. Wageni hawa na Wakongo wameshindwa, akiwemo kiongozi wao," msemaji Sylvain Ekenge alisema.
Hakutaja ikiwa hii ilimaanisha walikuwa wamezuiliwa au kuuawa.
Tina Salama, msemaji wa Rais Felix Tshisekedi, pia alithibitisha kwa shirika la habari la Reuters kwamba ikulu ya rais ilishambuliwa Jumapili asubuhi lakini jeshi lililikuwa limechukua udhibiti tena.
Hapo awali, walinzi wawili na mshambuliaji mmoja waliuawa katika shambulio dhidi ya nyumba iliyo karibu ya Vital Kamerhe, mbunge ambaye anatarajiwa kuwa spika, msemaji wa Kamerhe na balozi wa Japan walisema kupitia jumbe za mtandao wa kijamii wa X.
Ubalozi wa Marekani ulitoa tahadhari ya usalama siku ya Jumapili ukionya kuhusu "shughuli zinazoendelea kufanywa na maafisa wa usalama wa DRC" na ripoti za milio ya risasi katika eneo hilo.
Ukurasa wa Facebook unaoonekana kuwa wa Christian Malanga, mwanasiasa anayeishi Marekani, ulichapisha video ya moja kwa moja ambayo alionekana kuongoza mashambulizi hayo.
"Sisi, wanamgambo, tumechoka. Hatuwezi kuendelea na Tshisekedi na Kamerhe, wamefanya mambo mengi ya kijinga katika nchi hii," alisema kwa Lingala kwenye video hiyo, ambayo haijathibitishwa na Reuters.
Tshisekedi alichaguliwa tena kwa muhula wa pili kama rais mwezi Disemba, lakini bado hajaunda serikali, wiki sita baada ya kumteua waziri mkuu.
Kamerhe alikuwa mgombea wa spika wa bunge katika uchaguzi ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Jumamosi lakini ukaahirishwa na Tshisekedi. - Reuters
#mapinduzi #drc #jeshi #wanamgambo #felixtshisekedi #voa #voaswahili