Idadi ya vifo katika eneo la kutupia takataka vyafikia 21

  • | VOA Swahili
    219 views
    Polisi wa Uganda wamesema Jumapili kuwa idadi ya vifo kutokana na maporomoko ya ardhi kwenye eneo kubwa la kutupia taka mjini Kampala imefikia 21, wakati timu za uokozi zikiendelea kutafuta manusura na idadi ya miili inayopatikana ikielekea kuongezeka. Kwa mujibu wa shirika la habari, mvua kubwa ambazo zimekuwa zikinyesha katika wiki za karibuni zilisababisha kuporomoka kwa sehemu ya eneo hilo, ambalo ndilo pekee linalotumika kutupa takataka mjini humo, na kupelekea kufunikwa kwa baadhi ya nyumba zilizokuwa karibu, wakati wenyewe walipokuwa wamelala. Mamlaka za jiji Jumamosi zilisema kuwa watu 8 walikufa, lakini kufikia leo idadi hiyo imeongezeka hadi 21, huku wengine 14 walijeruhiwa. Kati ya waliofariki miili isiyopungua miwili ilikuwa ya watoto. Shirika la Msalaba mwekundu nchini humo limesema kuwa mahema yamewekwa karibu na eneo la tukio, ili kutoa hifadhi kwa watu walioathiriwa. Eneo hilo linalofahamika kama Kiteezi, kwa miongo mingi limekuwa likitupwa taka taka za Kampala, hadi kugeuka na kuwa mlima, huku wakazi waishio karibu wakilalamika kutokana na taka zenye sumu, pamoja na uharibifu wa mazingira. Nchini Ethiopia, takriban watu 115 walikufa 2017 baada ya eneo la taka mjini Addis Ababa kuporomoka, huku wengine 17 wakifa 2018, mjini Maputo, Msumbiji, kwenye tukio sawa na hilo. – Reuters, AP, VOA #uganda #kampala #takataka #dumpo #maporomoko #vifo #polisi #voa #voaswahili