Nchini Malawi ambako kuthibitisha habari sahihi kumejaa changamoto, Taasisi ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika MISA inafanya kazi ili kuboresha usahihi wa kuripoti na kuwasaidia waandishi wa habari kujenga uaminifu.
Gazeti la The Nation
Suzgo Chitete ni mwandishi wa habari za uchunguzi na naibu mhariri mkuu wa gazeti la kila siku la Malawi, The Nation, huko Lilongwe. Kila asubuhi anafika kazini akiwa na imani kwamba uandishi wa habari ni wito wa kutoa taarifa za ukweli kwa wasomaji.
Chitete na waandishi wengine kadhaa wa habari nchini Malawi walihudhuria mfululizo wa mafunzo yanayoangazia ukweli ambayo yanawapa waandishi wa habari ujuzi wa kugundua habari potofu na habari zisizo za kweli.
Suzgo Chitete, Mwandishi wa gazeti la The Nation anaeleza: "Mafunzo haya yameleta mwamko na kutukumbusha kwamba kila tunapoandaa habari, au kila wakati tunapofanya mahojiano na mtu, lazima tuwe makini na taarifa za uongo, ili wasikilizaji wapatiwe taarifa za kuaminika."
Taasisi ya Vyombo vya Habari MISA
MISA Malawi, bodi ya ndani katika Taasisi ya Vyombo vya Habari ya Kusini mwa Afrika, inaendesha programu hizi kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya kimataifa. Mpango wake unaowapatia waandishi wa habari ujuzi wa kuhakiki habari za kweli, unaungwa mkono na Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Habari cha Deutsche Welle. Mwenyekiti wa MISA nchini Malawi, Golden Matonga anaelezea.
Golden Matonga, Mwenyekiti wa MISA Malawi: "Tuna DW Akademie ya Ujerumani ambayo imekuwa ikisaidia kazi zetu za msingi katika MISA Malawi kwa misingi ya kujenga uwezo wa miradi kwa waandishi wa habari wa Malawi. Tunashirikiana na UNESCO kuangalia kusaidia ripoti za uchaguzi kwa ujumla ambapo pia imewezesha kufikia maeneo ya kuangalia ukweli kuhusu taarifa."
Matonga anasema mradi wa Elimu ya Uandishi wa Habari wa MISA Malawi unatoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa Malawi ili kuzuia kuenea kwa taarifa potofu na za uongo ambazo ni muhimu hasa wakati nchi inapojiandaa kwa uchaguzi mkuu 2025.
Golden Matonga, Mwenyekiti wa MISA Malawi anasema: Hivi karibuni tulishuhudia kifo kibaya cha makamu wa rais na kuna habari nyingi za uongo ambazo zilisambaa kuhusu kile kilichotokea katika ndege iliyoanguka. Matukio haya yanatukumbusha jinsi habari za uongo zinavyoweza kuwa hatari. Tunaelekea kwenye uchaguzi. Hapo awali tulikuwa na uchaguzi wa wabunge 2019 na uchaguzi wa rais 2020. Kisha tukaanza kuona tena mwenendo wa habari za uongo zinazoathiri nafasi ya kisiasa.
Ukweli wa Wanasiasa
Maeneo ya kuzingatia ni pamoja na kuangalia ukweli wa wanasiasa, na madai yanayohusiana na uchaguzi, na kuthibitisha maudhui ya vyombo vya habari kama vile picha na video kwa kutumia zana kama vile Google Image Search.
Ripoti ya Mwandishi wa VOA Lameck Masina kutoka Lilongwe, Malawi.
#habaripotofu #malawi #lilongwe #waandishi #habari #MISA #kusinimwaafrika #usahihi #uaminifu #voa #voaswahili